WANANCHI Wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki na ulinaji asali Wilayani Njombe, Iringa,wameiomba Serikali kupitia sekta ya Mali Asili na Utalii nchini, kuwasaidia kutangaza soko la bidhaa hiyo, pamoja na kuwatambua kisheria ili kuruhusu watalii kutoka nje na ndani ya nchi kutembelea vituo vyao kujionea shughuli wanazo zifanya ili kutangaza soko la bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi.
Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti Wilayani humo,wafugaji hao walisema ufugaji nyuki ni kitengo ambacho kama kikipewa kipaumbele inaweza kuliingizia pato pato taifa na hata wananchi wenyewe kwani wanunuzi ni wengi isipokuwa hakuna jitihada za kuitambulisha bidhaa hiyo kitaifa na kimataifa.
Bw. Tobias Gadau mkazi wa Mji mdogo wa Makambako, ni mfugaji ni mmoja kati ya wafugaji wengi ambao Majira lilifanikiwa kutembelea maeneo ambayo anafanyia kazi ya ufugaji nyuki na uvunaji asali ambaye amefuga mizinga zaidi ya 250 ya nyuki ambayo ipo katika shamba lenye ekari 7.
Bw. Gadau alisema kinachokwamisha maendeleo ya kazi hiyo ni urasimu uliopo katika serikali na ugumu wa soko ambapo licha ya kuwa na bidii katika kutafuta soko amekuwa akikwama kwani hakuna jitihada zinazofanywa na serikali kutangaza kuwepo kwao na kwamba wanunuzi hutegemeana na utambulisho ambao serikali ilipaswa kuwasaidia kuwatambulisha ili kukuza soko la asali nchini.
Alisema, amekuwa akipokea wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali za nchi ambao hushangaa mazingira hayo yalivyo na kwamba wengi wao husema shamba hilo ni kivutio tosha kwa watalii ambao wangeweza kuwa wanunuzi wa zao hilo na kwenda kulitangaza soko mahali pengine.
Bw. Gadau alisema wageni wengine waliofanikiwa kutembelea shamba hilo ni wageni kutoka nchi tano za Uholanzi,Mrekani na nchi jirani za Malawi, zambia na Kenya, ambao wengi wao wanaifurahia asali ya Tanzania na kusifia kuwa hawajapata asali kuona mahali popote ambapo wamewahi kutembelea.
Alisema licha ya kuwa asali ni bidhaa inayohitajika wamekuwa wakiishia kuuza kwa kutembeza mitaani na mara nyingine kwa wageni ambao baada ya kutambua ubora wa asali hiyo,na kwamba wamenufaika na asali hiyo kwani wengine wanaofahamu faida za asali wanatumia kama tiba ya malazi mbalimbali ambayo baadhi yake yameshindikana kutibika kitaalamu.
Alieleza tangu aanze kufuga nyuki mwaka 1998 hadi sasa amekuwa akipata watu ambao wanahitaji elimu juu ya ufugaji, ulinaji asali pasipo kuharibu mazingira na jinsi ya kuhudumia nyuki pasipo kuwapa madhara yoyote, na kwamba faida ambazo amepata katika kazi hiyo ni pamoja na kuweza kununua mashamba na kupanda miche 1,225,000,katika eneo la ekari zaidi ya 100.
Uvunaji wa asali alisema ni mara mbili kwa mwaka na kwamba huvuna zaidi ya ndoo 15 ambapo huweza kuingiza kiasi cha fedha hadi sh. milioni 3.05 ambapo hutegemea wanunuzi kutoka katika mikoa ya Mbeya, Dare es salaamu, Morogoro na Iringa yenyewe.
Mwisho.